fbpx

Kwanini tujadili kuhusu ugonjwa wa figo?

Magonjwa ya figo yameongezeka kwa kasi sana duniani. Kunasababu nyingi zinazopelekea magonjwa hayo lakini kisukari na shinikizo la damu yanaongoza.Magonjwa yasiyoambukiza hasa kisukari na shinikizo la damu yanasababisha kwa kiasi kikubwa magonjwa ya figo.

Sukari ikiwa nyingi kwenye damu husababisha mishipa midogo ya damu kwenye figo kuharibika na kupelekea magonjwa ya figo.

Shinikizo la damu linashika nafasi ya pili baada ya kisukari kwenye kusababisha magonjwa ya figo. Hii hutokea baada ya shinikizo la damu kuongezeka kutokana na kukakamaa kwa mishipa midogo ya damu ya figo. Mara nyingine shinikizo la damu huja baada ya magonjwa ya figo au kinyume chake.

Watu wenye kisukari pamoja na shinikizo la damu wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya figo,hivyo ni muhimu kujua namna nzuri ya kujikinga na kutahadhari na magonjwa ya figo.

Kwenye Makala hii utapata maelezo kuhusu magonjwa ya figo,dalili zake,vipimo na matibabu yake. Pia utapata kujua namna ya kujikinga na magonjwa ya figo yanayozuilika.

Kwani figo nini?

Figo ni moja ya kiungo cha mwili kilichopo sehemu ya juu  na nyuma ya tumbo. Zipo pande mbili za uti wa mgongo.  Figo zipo jozi zinaumbo la harage.

Ni zipi kazi za figo?

Kazi kuu ya figo ni kusafisha damu. Kuondoa vitu visivyofaa,chumvi chumvi na kemikali nyingine kwa njia ya mkojo.

Kazi nyingine ni,

  • Kutoa maji yaliyozidi mwilini ili kuweka sawa kiasi cha maji kulingana na mahitaji ya mwili.
  • Kusawazisha madini na kemikali mwilini.
  • Kuchunga shinikizo la damu kwa kuweka sawa kiasi cha madini mwilini. Pia huzalisha homoni zinazosaidia kuweka sawa shinikizo la damu.
  • Kuzalisha chembe hai nyekundu za damu.
  • Kuimarisha mifupa kwa kubadilisha vitamini D ili itumike kunyonya kalsiam kwenye chakula. Kalsiam ambayo ndiyo inayokuza na kuimarisha mifupa.

 

MAGONJWA YA FIGO.

Je niko kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa figo?

Mtu yeyote anaweza pata magonjwa ya figo. Hatari ya kupata magonjwa hayo inaongezeka pale mtu anapokua na;

  • Umri Zaidi ya miaka 60.
  • Ugonjwa wa kisukari.
  • Shinikizo la juu la damu.
  • Kutumia tumbaku.
  • Uzito mkubwa.
  • Matumizi ya mda mrefu ya dawa za kutuliza maumivu.

Dalili za magonjwa ya figo.

Dalili kuu ya magonjwa ya figo ni kuvimba mwili,hasa figo inaposhindwa kufanya kazi. Mara nyingi mgonjwa huvimba viungo vilivyopo mbali na moyo kama miguu na mikono. Mgonjwa anaweza vimba uso,tumbo na sehemu yoyote nyingine ya mwili.

Dalili nyingine ni,

  • Kuongezeka kwa shinikizo la damu kutokana na ukinzani kwenye mishipa midogo ya damu ya figo.
  • Upungufu wa damu. Baada ya seli hai nyekundu za damu kushindwa kuzalishwa na figo.
  • Kukosa hamu ya kula,kichefuchefu na kutapika.
  • Shida kwenye mkojo. Kukojoa mara kwa mara,mkojo kutoka kidogo,muwasho wa mkojo na ugumu wakati wa kukojoa.
  • Kupata maumivu juu ya kiuno,mgongoni yanayoelekea kwenye uti wa mgongo.

Kumbuka; dalili hizi ni za jumla,hutofautiana kati ya mtu na mtu. Dalili hizo pekee hazitoshi kujulisha kua una magonjwa ya figo. Ni muhimu kupata vipimo husika ili kugundua kama ni magonjwa ya figo au laa.

Vipimo gani hufanywa kugundua ugonjwa wa figo?

Kuna vipimo tofauti vinavyoweza kufanyika ili kugundua kama unaumwa mwagonjwa ya figo.

1. Kipimo cha mkojo.

Kipimo cha mkojo huweza kujulisha hali ya figo.

Kuwepo kwa vitu visivyo vya kawaida kwenye mkojo hua na maana.

  • Uwepo wa protini kwenye mkoja huashiria ugonjwa sugu wa figo. Wakati mwingine huashiria ugonjwa wa moyo.
  • Uwepo wa usaha kwenye mkojo uashiria uambukizo kwenye mfumo wa mkojo.
  • Protini na chembe hai nyekundu kwenye mkojo hutoa vidokezo vya ugonjwa wa uvimbe kwenye figo.

2. Kipimo cha damu.

Vipimo vya damu pia huweza kutambua magonjwa mbalimbali ya figo.

Kreatenin na urea.

Kipimo kikubwa kinachofanywa kwenye damu ili kuangalia utendaji kazi wa figo ni kreatinini (seram createnine). Kwa kawaida kreatenine ni uchafu unaotolewa kwenye damu na figo. Uwepo wa uchafu huo kwenye damu kwa kiasi kikubwa huashiria ugonjwa wa figo. Uchafu mwingine unaotolewa kwenye damu ni urea.

Himoglobini.

Kwa kua chembe hai nyekundu za damu zinazalishwa kwenye figo na ndizo ambazo zinabeba himoglobin,chembe hizo zikiwa chache ni dalili muhimu ya ugonjwa sugu wa figo.

Vipimo vingine vyenye kujulisha uwepo wa magonjwa ya figo kwenye damu ni;

  • kiwango cha Sukari kwenye damu
  • Kemikali madini – Electrolytes (sodiamu,potasi na klorini)
  • Kalsiam na madini mengine kwenye damu.

3. Vipimo vya radiologia.

Picha ya ultrasound ya figo.

Kipimo hiki husaidia kuona umbo la figo kama ni kubwa au wastani. Huonesha pia hali ya figo kama kuna maji au uvimbe wowote. Kipimo hiki hugundua kama kuna sehemu imeziba kwenye figo au ogani nyingine kwenye mfumo wa mkojo. 

Vipimo vingine vya radiologia ni;

  • X ray ya tumbo. Hujulisha uwepo wa mawe kwenye figo.
  • CT scan pia huweza kutumika kama kutakua na hatari ya uwepo wa magonjwa sugu ya figo.

 

Kuna aina ngapi ya ugonjwa wa figo?

Figo kushindwa kufanya kazi. (Kidney failure).

Figo inaposhindwa kufanya kazi yake ya kuchuja na kutoa uchafu kwenye damu. Kuweka sawa  electrolyti mwilini. Ugonjwa huu hua na sifa ya uwepo wa protini nyingi kwenye damu. Ugonjwa huu umegawanyika sehemu mbili:

Figo kushindwa kufanya kazi ghafla.(acute kidney injury)

Hali hii hutokea kwa pale ambapo figo ilokua inafanya kazi vizuri,ufanisi kupungua kwa haraka. Husababishwa na kuhara,kutapika,malaria kali,shinikizo la juu la damu nakadhalika.

Ugonjwa sugu wa figo. (Chronic kidney injury)

Hua na sifa ya figo kuanza kupoteza ufanisi wake kidogokidogo kila siku. Hali hiyo huweza dumu kwa muda mrefu bila kuonesha dalili. Pamoja na kuonesha dalili za awali za figo kushindwa kufanya kazi. Ugonjwa sugu wa figo hautibiki. Na ukifika hatua ya mwisho,figo husafishwa kwa dialisisi. Kubadilisha figo ndio nje pekee na ya muda mrefu kwa ugonjwa sugu wa figo.

 

Magonjwa mengine ni;

Maambukizi kwenye mkojo (UTI) – Ugonjwa huonekana kwa mkojo kua na usaha. Matumizi ya dawa ya kuua wadudu huponesha ugonjwa huu. Kama unajirudia mara kwa mara ni vizuri vipimo zaidi vikafanyika ili kubaini visababishi.

Uvimbe kwenye nephroni (nephrotic syndrome).- Ugonjwa huu huwakumba watoto zaidi kuliko watu wazima. Hutibiwa kwa dawa na kupona. Wakati mwingine huweza kujirudia rudia.

Mawe kwenye figo.(kidney stones) – Kukusanyika kwa madini kwenye figo husababisha kuundwa kwa vitu vigumu ambavyo hushindwa kutoka kwenye mkojo kwa urahisi. Mkusanyiko huo hutokana na matumizi duni ya maji. Mgonjwa anaweza hisi kichefuchefu,homa na kutapika.

 

Kuna tiba ya ugonjwa wa figo?

Kuna matibabu tofauti tofauti kulingana na aina ya ugonjwa unaoishambulia figo. Magonjwa hayo yameganyika sehemu kuu mbili.

Magonjwa yanayohitaji matibabu ni:

Hitilafu ya figo,maambukizi ya mfumo wa mkojo hutibiwa kwa dawa.

Lakini ugonjwa sugu wa figo unahitaji kusafishwa figo kwa dayalisisi na wakati mwningine kubadilisha au kupandikiza figo.

Magonjwa yanayohitaji upasuaji.

Ugonjwa wa mawe kwenye figo,kuziba kwa mfumo wa mkojo kwa namna yoyote ile unahitaji upasuaji. Hata saratani ya mfumo wa mkojo pia husaidika kwa upasuaji.

Nawezaje kujikinga na ugonjwa wa figo?

Unaweza kujikinga na magonjwa ya figo kwa kufanya yafuatayo;

1. Kunywa maji ya kutosha

Matumizi ya maji ni njia muhimu kwenye kujikinga na magonjwa mengi ya figo. Matumizi ya maji hutofautiana kati ya mtu na mtu kulingana na uzito wa mhusika. Kwa wastani mtu mzima anapaswa kunywa maji lita 3 kwa siku. Hii husaidia kuongeza ufanyakazi wa figo na kuzuia mawe kwenye figo. Husaidia pia kuzalisha mkojo mwingi ambao husafisha njia ya mkojo na kuzuia uambukizo kwenye njia ya mkojo.

2. Dhibiti sukari na shinikizo la juu la damu

Kwa kua magonjwa hayo mawili yanasababaisha magonjwa ya figo, inapaswa kupambana nayo. Kwa mgonjwa anaeugua magonjwa hayo,anapaswa kufuatilia tiba pamoja na kuhakikisha sukari na shinikizo la damu vinakua kwenye wastani wake.

3. Epukana na vihatarishi vya magonjwa ya figo

Fanya mazoezi ilia kupunguza uzito. Kupunguza au kuacha  uvutaji wa tumbaku na matumizi ya mazao ya tumbaku kwa kua vinaongeza hatari ya kupata magonjwa ya figo. Matumzi ya dawa za maumivu mara kwa mara uepukwe kama kutakua hakuna sababu ya muhimu.

4. Lishe bora

Mlo uliotimia husaidia kuboresha mwili na kuufanya utendaji kazi wake uwe sawia. Matumizi ya mbogamboga na matunda husaidia kuboresha afya ya figo na viungo vingine vya mwili. Pia husaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu.

Hitimisho

Magonjwa ya figo huua kimya kimya. Yanaweza kusababisha kuendelea kwa kupotea kwa kazi ya figo na kuelekea kwa hitilafu ya figo na hatimae kuhitaji dayalisisi au kubadilisha kwa figo ili kudumisha maisha.

Kwa sababu ya gharama kubwa na shida za kupatikana katika nchi zinazoendelea asilimia 5-10% ya wagonjwa wa hitilafu ya figo hupata matibabu kama dayalisisi na kubadilisha figo, wakati waliobaki hufa bila kupata tiba.

Ugonjwa sugu wa figo ni tatizo kubwa sana na hauna tiba, kwa hiyo kinga ndio njia pekee. Ugunduzi na matibabu ya mapema  huweza kuzuia hali ya ugonjwa sugu wa figo kuwa mbaya sana, na huweza kuzuia au kuchelewesha hata haja ya dayalisisi au kubadilisha/ kupandikizwa figo.

Kwa Makala Zaidi juu ya kujikinga na magonjwa mbalimbali tembelea tovuti yetu ya www.afyatechtz.com. Pia jipatia vifaa tiba vitakavyokusaidia kuweka afya yako salama ukiwa nyumbani kwako.

 

 

Shopping Cart
Muulize Dr. Adinan
1
Muulize Dr. Adinan
Chat na Dr. Adinan
watumie na wengine