Madhara ya Presha kwenye Moyo
Shinikizo la damu la juu, au kama linavyojulikana sana presha, linaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya moyo na kusababisha matatizo mbalimbali.
Presha inapokuwa juu huleta ukinzani na kusababisha moyo kufanya kazi ya kusukuma damu kwa kutumia nguvu zaidi, hivyo kuongeza hatari ya kuendeleza magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Baadhi ya matatizo yanayoweza kusababishwa na presha kwenye moyo ni kama yafuatayo:
1. Ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo
Presha inaweza kusababisha mishipa inayosambaza damu kwenye moyokukakamaa na kuwa membamba zaidi . Mishipa ya damu kuwa myembamba, inaweza kupunguza mtiririko wa damu kwenye misuli ya moyo, hivyo kusababisha maumivu kifuani (angina), mashambulizi ya moyo, matatizo yanayoweza kuwa hatari kwa maisha.
2. Moyo kuwa mkubwa
Kazi kubwa ya kusukuma damu ambayo moyo hufanya kwasababu ya presha inaweza kusababisha misuli ya moyo kuwa mikubwa. Hii ni kama kwa watunisha misuli, misuli yao huongezeka kadiri wanavyonyanyua uzito mkubwa.
Tofauti ya ukuaji wa misuli ya moyo huathiri uwezo wa moyo kusukuma damu kwa ufanisi. Matokeo yake moyo hushindwa kufanya kazi vizuri, mapigo ya moyo, na kuongeza hatari shambulio la moyo.
3. Moyo kufeli
Presha isiyodhibitiwa inaweza kusababisha moyo kufanya kazi kwa nguvu zaidi na kupoteza uwezo wake wa kusukuma damu kwa ufanisi. Maana yake ni kwamba kama moyo utashindwa kusukuma damu kwa kiwango kinachotakiwa, hautaweza kupokea damu kwa kiwango kinachotakiwa.
Hivyo, damu inayotoka sehemu mbalimbali za mwili zitaendelea kurundikana → Damu inaporundikana mishipa huvuja ili kupunguza kiwango cha maji kwenye damu. Maji haya huenda wapi? Maji haya huwenda kwenye sehemu zingine za mwili na kusababisha uvimbe.
Sasa umeelewa kwanini ambao wana ugonjwa wa moyo kufeli huvimba miguu, tumbo na sehemu zingine ambazo hatuzioni. Wakati mwengine huambiwa mapafu yamejaa maji. Hichi ndicho hutokea.
Kulingana na sehemu maji yalipokusanyika, mgonjwa ataonesha dalili kama vile kukosa pumzi, uchovu, kuvimba tumbo, na kushindwa kutembea, kukosa hamu ya kula, na hata kukonda.
4. Matatizo ya mapigo ya moyo
Presha inaweza kuvuruga shughuli ya kawaida ya umeme katika moyo, hivyo kusababisha mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida (matatizo ya mapigo ya moyo).
Matatizo haya ya mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida yanaweza kuongeza hatari ya matatizo kama vile kuganda kwa damu, kiharusi, na kukamatwa kwa moyo ghafla.
5. Mshtuko wa Moyo
Shinikizo la damu la juu (presha) linachangia katika maendeleo ya atherosclerosis, hali inayojulikana kwa kujengeka kwa utando kwenye mishipa ya damu.
Iwapo utando utabandukana kuziba njia ya damu kwenye mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye moyo, inaweza kusababisha mshtuko wa moyo (heart attack).
Shambulio au mshtuko wa moyo hutokea pale misuli ya moyo inapokosa damu ya kutosha.