fbpx

Nyama na presha vinahusiana?  Nyama ni tamu. Na kwa waliozooea kuiacha ni ngumu? Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu athari za kula nyama. Nami licha ya kuwa daktari nilipitia changamoto hii.

Baada ya kupitia tafiti nyingi za kutosha zilizofanya ndani na nje ya nchi nimeona nikuandikie makala haya yatakayokujibu masuali mengi uliyonayo kuhusu nyama.

Hatahivyo nikutoe hofu. Nyama siyo hatari, bado unaweza kuendelea kula, kuenjoy bila kupata madhara yeyote.

Katika makala haya nitakufahamisha kwanini nyama inaweza kuleta madhara, ni nyama za aina gani zinazoweza kukuletea madhara. Pia nitakufahamisha kuhusu upendelee kula aina gani ya nyama na kwanini.

Sintoishia hapo bali nitakupa ushauri kuhusu kiwango na namna ya kuandaa nyama yako kwa afya bora. Kama unapenda supu, pia nimegusia kidogo.

Sasa tuendelee. Lakini kwanza ngoja, tufahamu umuhimu wa nyama mwilini. 

Umuhimu wa Nyama Kwa Afya Yako

Tangu jadi vyanzo vya nyama vimekuwa ni wanyama tunaofuga wa miguu minne, wanyama jamii ya ndege na samaki.

Hatahivyo kwa technologia kuendelea, sasa hivi kuna nyama zinazotengenezwa maabara.

Nchi ambazo zimeruhusu matumizi ya nyama zilizotengenezwa maabara mpaka sasa ni Marekani, Uingereza, Australia.

Lakini nyama ni muhimu au tunajilia tuu? Eti mwenzangu, unajua umuhimu wa nyama?

Nyama ina umuhimu mkubwa katika mwili wetu kutokana na faida kadhaa za lishe.

Hapa chini ni baadhi ya umuhimu wa nyama mwilini:

  1. Nyama ni chanzo cha Protini: Nyama ni chanzo bora cha protini. Protioni ni muhimu kwa ujenzi na ukarabati wa mwili, ikiwa ni pamoja na misuli, ngozi, na mfumo wa kinga. Protini pia husaidia katika kudumisha afya ya mfumo wa kinga na kuzalisha kemikali na homoni.
  2. Nyama ina Madini na Vitamini: Nyama ina madinni muhimu kama vile zinki, chuma, na fosforasi. Vitamini tunazozipata kutoka kwenye nyama ni vitamini B12, vitamini B6, riboflavin, na niacin. Madini haya na vitamini ni muhimu kwa afya ya mfumo wa mishipa ya fahamu, utengenezaji wa nishati, umeng’enyaji wa chakula, na utengenezaji wa seli nyekundu za damu.
  3. Nyama ni chanzo cha Amino Acid: Amino acid ni chembe ndogondogo zinazotumika kutengeneza protini. Nyama ina amino asidi muhimu ambazo mwili hauwezi kuzalisha kwa wingi. Amino acid hizi ni kama vile leusini, isoleusini, na valini. Amino acid hizi ni muhimu kwa ujenzi wa misuli, kudumisha afya ya ngozi, na kusaidia katika mchakato wa kupona baada ya kuumia.
  4. Chanzo cha Nishati: Nyama pia ina mafuta, ambayo ni chanzo kikuu cha nishati katika mwili. Mafuta yanatoa nguvu zinazohitajika kwa shughuli za kila siku na kudumisha kiwango cha juu cha utendaji mwilini.

Nile Nyama Ya Aina Gani Kudumisha Presha na Afya Yangu?

Kuhusu aina ya nyama, ni muhimu kuchagua nyama zenye kiwango cha chini cha mafuta. Kama unapenda yale mafuta yanayozima moto, kwasasa punguza mpaka uache kabisa.

Chaguzi bora ni pamoja na:

  1. Nyama ya kuku: Pendekezo ni kula kuku bila ngozi –  ili kupunguza ulaji wa mafuta yasiyo na afya.
  2. Samaki: Samaki kama vile samaki wa maji baridi kama salmon, sardini, na tuna wana wingi wa asidi ya mafuta omega-3 ambayo ina faida kwa afya ya moyo na inaweza kusaidia kudhibiti presha ya damu.
  3. Nyama isiyo na mafuta: Chagua sehemu za nyama zisizo na mafuta mengi, na nyama pori. Kwenye nyama pori hakikisha una kibali au umenunua kwenye maduka yanayotambulika kisheria. 

 

MUHTASARI

Epuka kutumia nyama zenye mafuta mengi kama nyama nyekundu iliyonona au nyama iliyokaangwa kwa mafuta mengi.

Nile nyama kiasi gani kwa siku?

Aya hii huwenda ikawa ngumu kwako kuelewa. Sinto kushangaa na hautokuwa mwenyewe. Tuko wengi hapa. Haswa kama wewe huridhiki mpaka ule kilo moja na nusu ya nyama kila ukiona moshi.

Rafiki yangu hupenda kusema, tule nyama mpaka tuote tunakula majani kama ng’ombe.

Nachotaka kukwambia ni kwamba, kwasiku unahitaji kiwango kidogo tu cha nyama.

Kwa kawaida, tunahitaji angalau finyango nne za size ya kawaida ya nyama kwa siku. Kwa vipimo ni gramu 85-115 za nyama iliyopikwa kwa siku au nusu kilo mpaka robo tatu kilo kwa wiki. 

Huwezi amini! Naelewa.

Lakini kama unapenda kula zaidi ufanyaje? Kuna namna. Inabidi uweze kuchagua nyama nzuri kwa afya yako. Rejea aina za nyama

Nyama Nyekundu Inashida Gani?

Kama tulivyoona kwenye makala kuhusu vyakula kwa mgonjwa wa presha, aina na kiwango cha chakula kinaweza kuathiri presha yako. 

Tafiti zinaonesha kwamba nyama nyekundu zinaongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ikilinganishwa na nyama nyeupe.

Utafiti uliofanywa na Havard umeonesha kwamba watu wanaokula nyama nyekundu wamekuwa na lehemu mbaya ukilinganisha na wale wanaokula nyama nyeupe au wale wanaokula protini kutoka katika vyanzo vya mimea. 

Utafiti mwengine umeonesha kwamba ulaji wa nyama nyeupe kupunguza hatari ya mtu kupata viashiria vya magonjwa ya moyo.

Hatahivyo ifahamike kwamba athari ya nyama nyekundu kwenye afya ni kutokana na mafuta yaliyopo kwenye nyama hiyo na si nyama yenyewe.

Maswali kuhusu njia ya upikaji wa nyama 

  • Nyama ya Kuchoma (Grilling): Upikaji wa nyama kwa kuchoma kunaweza kuwa chaguo nzuri, haswa ikiwa unapika nyama bila kuongeza mafuta mengi. Ni vizuri kuondoa ngozi ya kuku kabla ya kuchoma ili kupunguza kiwango cha mafuta.
  • Nyama ya Kukaanga (Frying): Upikaji wa nyama kwa kukaanga unaweza kuongeza kiwango cha mafuta katika chakula chako. Ikiwa unapenda kukaanga, tumia mafuta yenye afya kama vile mafuta ya alizeti kiasi kidogo. 
  • Nyama ya Kuchemsha (Boiling): Kuchemsha ni njia nyingine ya kuandaa nyama bila kuongeza mafuta. Unaweza kuchemsha nyama kwenye maji tui au kuongeza viungo vya ladha kama vile vitunguu, tangawizi, au mimea mingine ili kuongeza ladha. Hatahivyo inabidi kuzingatia unywaji wa supu ili kuepuka mafuta mengi yaliyotoka kwenye nyama.

Ni muhimu pia kuzingatia njia za upikaji zisizo za mafuta kama vile kupika nyama kwa kutumia oveni au kupika kwa mvuke. Kwa kuongezea, epuka kutumia nyama zenye mafuta mengi kama nyama nyekundu iliyonona au nyama iliyokaangwa kwa mafuta mengi.

Vipi, nawe ulikuwa unahofia kula nyama? Tuambie tafadhali kwa kutuandikia hapo chini

 

SAIDIA WENGINE

  • Tutafurahi kusikia maswali au maoni yako kuhusu makala haya. Tafadhali tuandikie hapo chini.
  • Tafadhali Like na Kusambaza Ujumbe Huu Kwa Watu Unaofikiri Watanufaika na Ujumbe Huu.
 
Shopping Cart
Muulize Dr. Adinan
1
Muulize Dr. Adinan
Chat na Dr. Adinan
Muulize Dr. Adinan