Madhara ya Kisukari: Kinywa na Meno
Ugonjwa wa Kisukari husababisha kiwango cha sukari kuwepo kwa wingi katika damu na hivyo katika mate yako. Bakteria walioko mdomoni hutumia sukari hii kama chakula. Kwa hiyo bakteria hukuwa na kustawi zaidi katika mazingira yenye sukari. Bakteria hawa husababisha meno kuoza na kutoboka. Na kama hujapata tiba haraka unaweza kupoteza jino kwa kung’oa.
Kumbuka tulisema kisukari hupunguza kinga ya mwili kwa kuharibu seli nyeupe. Seli nyeupe hukusaidia kupambana na magonjwa kwa kuwakamata na kuwaharibu bakteria wanapoingia kwenye mwili.
Unaweza kupata changamoto zifuatazo mdomoni kama una kisukari
- Kukauka kwa mate
- Vidonda visivyopona haraka mdomoni
- Fizi kuoza na kutoka damu kirahisi\
- Meno kuoza na kutoboka
Namna ya kuwa na afya bora ya kinywa na meno
Kudhibiti sukari ni silaha yako muhimu. Unapodhibiti sukari pia hukuwezesha kudhibiti magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.
Hakikisha unapata huduma kutoka kwa mhudumu wa afya pindi utakapokuwa na dalili zifuatazo
- Fizi kuwa nyekundu kuliko kawaida ulivyozoea
- Fizi kutoka damu kwa urahisi
Piga mswaki angalau mara mbili kwa siku na kutumia fluoride.