Kisukari huathiri mishipa ya fahamu. Hatahivyo unaweza kuepuka kwa kufanya yaliyoshauriwa kwenye makala haya. Kisukari huweza kuleta uharibifu wa aina nne kwenye mishipa ya fahamu. Unaweza kuwa na aina zaidi ya moja. Dalili hutegemea aina ya uharibifu na mshipa wa fahamu ulioathiriwa.
Mfumo wa mishipa ya fahamu: Aina za Mishipa Ya Fahamu
Mishipa ya fahamu ni mfano wa nyaya za umeme. Nyaya hizi hubeba ujumbe kutoka kwenye ubongo au uti wa mgongo na kuzipeleka kwenye viungo vya mwili. Pia hupeleka ujumbe kutoka kwenye viungo vya mwili na kuupeleka kwenye ubongo au uti wa mgongo. Kupitia ujumbe huu, ubongo huutambua, huchanganua na kamua mwili ufanye nini. Ukishaamua mwili ufanye nini basi taarfia hizi hupelekwa kwenye viungo husika ili kutekeleza kazi iliyokusudiwa.
- Mishipa mikuu: Ubongo na uti wa mgongo- kazi yake ni kupokea taarifa kutoka kwenye viungo mbalimbali vya mwili, kuzichambua na kuamua nini kifanyike. Utaamua nini cha kufanya kulingana na kumbukumbu zako au kulingana na hisia za mwili wako kuhusu kitu hali/kitu husika.
- Mishipa ya pembeni:
- Mishipa inayochomoza kutoka kwenye uti wa mgongo kuelekea sehemu inazohudumu
- Autonomic – hiii ni mishipa ya fahamu inayohudumia viungo ambavyo vinafanya kazi bila ridhaa yako. Kwa mfano, moyo kibofu cha mkojo, nembo ya jicho, viungo vya uzazi.
Ili kuelewa kwa urahisi kazi ya mishipa ya fahamu nitakupa mfano. Fikiria kwamba umeona mnyama mkali. Kutaka kumfukuza ili kujihami unaaangalia huku na kule kutafuta silaha. Unaona jiwe liko karibu. Unainama kuliokota lakini unahisi maumivu makali. Kumbe jiwe lilikuwa la moto sana kwasababu ya jua. Je, utafanyaje? Kama jibu lako ni utalitupa basi ubongo wako unafanya kazi vizuri.
Uliona mnyama, mishipa ya fahamu ikapeleka ujumbe kwenye ubongo. Ubongo ulivyotafsiri taswira ukakwambia huyu ni mnyama mkali hivyo inabidi ujihadhari na uchukue hatua mapema. Ubongo ukatuma ujumbe uliobebwa na mishipa ya fahamu ya pembeni na kusema kwamba uiname uokote jiwe. Mkono ukatuma ujumbe kwamba unaungua lakini pia kitu ulichoshika si cha thamani. Uti wa mgongo ukakuamuru -bila wewe kuamua-kutupa lile jiwe. Vipi ingekuwa umebeba almasi ya moto? Hahahhaha….
Kwasababu ubongo wako unafanya kazi vizuri, hali itakuwa kama vile unavyoepua mboga kutoka jikoni. Licha ya kuungua huwezi kuitupa. Au nakosea? Hivyo ndivyo ambavyo mishipa ya fahamu hufanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha unaishi kwa raha huku ukiweza kugundua hatari na kuchukua tahadhari muhimu.
Mfano mwengine. Kuna utani kwamba ukiwaona wale wanaopiga matarumbeta basi pita na limao. Kwa nini? Hii ni kama lengo lako ni kuharibu shughuli. Ukipita na limao kama kuna aliyewahi kula limao kati ya wapulizaji…mdomo utajaa nini….? Hapa ujumbe uliotumwa kutoka kwenye macho ni taswira iliyotafsiriwa na ubongo kuwa ni limao. Ubongo ushajua limao chachu, hivyo mwili unajiandaa kupunguza ukali wa limao kwa kutoa mate mengi.
Hadi sasa ushakuwa mtaalamu wa mishipa ya fahamu. Tusubiri somo linalofuata kuhusu madhara haya na dalili zake. Usiache kufuatilia, tutaelekeza mpaka tiba. Ila kama kawaida yetu, kidogo kidogo.
Aina ya Uharibifu wa Mishipa ya Fahamu
Kurahisisha uelewa, uharibifu wa kisukari kwenye mishipa ya fahamu umegawanywa katika makundi manne (4). Kisukari huweza kuleta uharibifu wa aina nne kwenye mishipa ya fahamu. Unaweza kuwa na aina zaidi ya moja ya uharibifu. Dalili hutegemea aina ya uharibifu na mshipa wa fahamu ulioathiriwa.
Makundi haya ni kama ifuatavyo:
- Uharibifu wa mishipa ya fahamu ya pembeni
- Uharibifu wa mishipa ya fahamu ya autonomiki
- Uharibifu wa mshipa mmoja mmoja wa fahamu
- Uharibifu wa mishipa ya fahamu ya karibu
Uharibifu wa mishipa ya fahamu ya pembeni
Uharibifu wa mishipa ya pembeni huathiri mikono na miguu. Wagonjwa wengi wa kisukari wamekuwa na madhara haya. Kwa kawaida dalili hizi huanza kwenye miguu yote au mmoja.
Kama mishipa ya fahamu ya pembeni imeathiriwa mgonjwa wa kisukari huanza kuhisi maumivu au ganzi kwenye miguu au mikono. Mgonjwa huhisi kama vile anachomwa na sindano au kupigwa miguu.
Wakati mwingine miguu huwa na hisia zilizozidi kiasi kwamba mtu anaweza kuhisi kama vile amevaa soksi, kumbe la. Wakati mwengine mgonjwa huhisi maumivu makali hata kama kilichomgusa ni shuka.
Dalili zingine zinaweza kujumuisha:
- Ganzi au udhaifu.
- Kupungua kwa hisia miguuni na hivyo kutokuweza kuhisi mkandamizo au mchubuko kwenye miguu.
- Hali ya kupungua kwa uwezo wa miguu kuhisi mabadiliko kwenye mguu husababisha vidonda kuwa vikubwa, maambukizi, na maumivu na kutokupona kwa haraka. Kukatwa miguu kwasababu ya kuwa na vidonda visivyopona na vyenye maambukizi imekuwa ni changamoto kubwa kwa wagonjwa wa kisukari. Jifunze jinsi ya kutunza miguu yako. (Kama unahitaji elimu hii, nitumie msg)
Uharibifu wa mishipa ya fahamu ya Autonomic
Mishipa ya fahamu ya autonomiki huudumia viungo ambavyo vinafanya kazi bila ridhaa yako. Viungo vinavyofanya kazi bila ridhaa yako ni moyo, kibofu cha mkojo, tumbo, utumbo, viungo vya uzazi, na macho pindi yanavyoitikia kichocheo cha mwanga. Dalili zinaweza kujumuisha:
Uharibifu katika mishipa ya fahamu inayohudumia moyo huweza kusababisha mgonjwa wa kisukari kutokugundua dalili za shambulio la moyo
Presha ya damu kushuka wakati unasimama. Mgonjwa atahisi kichwa chepesi na kizunguzungu wakati anaposimama. Hali hii hutokea wakati mishipa ya fahamu inayohudumia mishipa ya damu imeathirika Jifunze kuhusu presha ya damu ya kushuka.
- Matatizo ya kibofu ambayo yanaweza kusababisha kuvuja kwa mkojo.
- Matatizo ya tumbo ambayo yanaweza kusababisha kuvimbiwa, au kuharisha.Kichefuchefu, kupoteza hamu ya kula, na kutapika.
- Uoni hafifu unapotoka kwenye mwanga na kwenda gizani.
- Kupungua kwa uwezo wa muitikio wa viungo vya uzazi wakati wa kujamiiana: hii hujumuisha uume kushindwa kusimama au ukavu wa uke.
- Kupungua kwa hisia wakati wa kujamiiana (https://www.healthline.com/health/diabetes/can-diabetic-neuropathy-be-reversed#complications)
Uharibifu wa Neva wa Karibu
Kisukari kinapoathiri mishipa ya fahamu inayohudumia miguu, mapaja, viuno, au makalio huitwa proximal Neuropathy. Inaweza pia kuathiri eneo la tumbo na kifua. Dalili zinaweza kujumuisha:
- Maumivu makali kwenye nyonga na paja au kiuno.
- Shida ya kuinuka kutoka kukaa, wakati mwengine mgonjwa hawezi kuinuka bila msaada.
- Maumivu makali ya tumbo.
Proximal Neuropathy hutokea mara chache sana, angalau mgonjwa 1 kati ya wangonjwa 100(). Mara nyingi hutokea kwa wanaume wenye umri zaidi ya miaka 50. Na inaweza kutokea hata kwa mgonjwa ambaye amedhibiti sukari yake. Proximal Neuropathy huwa kali kwa muda kisha hupungua makali yake. Wagonjwa wengi wamekuwa wakipona kabisa hali hii kadri muda unavyokwenda.
Uharibifu wa Mshipa mmoja mmoja wa Fahamu
Kisukari pia huweza kuharibu mshipa mmoja wa fahamu unaohudumia kiungo husika. Inapotokea hali hii, kiungo kilie tu, au kazi ile tuu ambayo ulitegemea ifanywe na ule mshipa kitadhurika au haitafanyika. Uharibifu wa aina hii hutokea kwenye mshipa mmoja wa fahamu. Kwa mfano mikononi, kichwa, au mguu. Dalili zinaweza kujumuisha:
- Ganzi au kuchoma choma katika mikono au vidole.
- Kupoteza nguvu mkononi mwako unaoweza kukufanya udondoshe vitu ambavyo ulikuwa ukiweza kuvibeba hapo kabla.
- Shida ya kuona au kuona vitu viwili viwili
- Kutokuweza kuchezesha sehemu moja ya uso wako
- Maumivu nyuma ya jicho moja.
Tiba kwa mishipa ya fahamu iliyoathiriwa na Kisukari
Matibabu ya uharibifu wa mishipa ya fahamu yana malengo matatu (3);
- Kuzuia uharibifu usiendelee na kutokea
- Kudhibiti maumivu
- Kushughulikia madhara yaliyokuwepo.
Unahitaji kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Inashauriwa kuwa na sukari angalau 4 – 7 mmo/L kabla hujala na 7 – 10mmol/L masaa mawili baada ya kula. Kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu kutakusaidia pia kupoa kwa dalili zitokanazo na madhara yaliyojitokeza tayari kwasababu ya kisukari.
Kuna dawa aina nyingi zitumikazo ili kupoza maumivu kwa mgonjwa aliyepata athari kwenye mishipa ya fahamu kwasababu ya kisukari. Dawa hizi ziko katika makundi. Ni bora kushauriana na daktari wako ili kufahamu utumie aina ipi ya dawa na kwa wakati gani.
Kudhibiti au kushughulikia madhara ya kisukari yanajumuisha fani mbalimbali kulingana na madhara yenyewe yalipojitokeza. Kama tulivyoona, kisukari huathiri mfumo wa mkojo, mfumo wa usagaji wa chakula na hata mfumo wa uzazi. HIvyo, unashauriwa kuwasiliana na daktari wako kuhakikisha unapata tiba stahiki.