fbpx

Shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito

Facebook
Twitter
WhatsApp

Imeandikwa na Dr. Adinan J. MD. MSc. FDHS. F.Forgatty, mtafiti wa magonjwa na  mkufunzi wa vyuo vya Afya kwa zaidi ya miaka 10. 

UTANGULIZI.

Ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu kipindi cha mimba  umeongezeka kutoka milioni 16.30 mpaka milioni  18.08 duniani,ambayo ni ongezeko la asilimia 10.92 kutoka mwaka 1990 mpaka 2019.Tatizo hilo linaongoza kusababisha vifo na matatizo kwa akina mama wajawazito duniani. Miongoni mwa matatizo yanayotokana na shinikizo la juu la damu kipindi cha mimba ni kifafa cha mimba.

Tukusaidie Kudhibiti Presha?

Muulize Dr. Adinan sasa akushauri namna sahihi ya kudhibiti Presha. Utalipia TSh. 4900/= tu!

Tafiti zinaonesha kifafa cha mimba kinatokea kwa asilimia 2-8 kwa wajawazito wote, na kinachangia vifo kwa wajawazito kwa asilimia 9 barani afrika. Shinikizo la juu la damu hasa yanayopelekea kifafa cha mimba linasababisha vifo kwa akina mama wajawazito kwa asilimia 19 na kifafa cha mimba kinaripotiwa kua sababu namba mbili kwenye sababu zinazosababisha vifo kwa akina mama wajawazito Tanzania. Shinikizo la juu la damu linaweza kua limetokana na presha ya mda mrefu mbayo alikua nayo mwanamke kabla ya kupata ujauzito au shinikizo hilo linaweza kuongezeka kipindi cha ujauzito baada ya wiki ya 20 ya mimba kwa mwanamke ambae hapo kabla hakua na tatizo hilo.

Matatizo yanayotokana na shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito yanasababisha madhara moja kwa moja kwenye mimba na mama mwenyewe. Lakini pia husababisha madhara ya mda mrefu kama tatizo la moyo kua mkubwa na kushindwa kufanya kazi.

Tatizo hili linatibika kama mama mjamzito atawahi kugundulika kipindi cha mahudhurio ya kliniki ya ujauzito. Na kwa mwanamke mwenye shinikizo la juu la damu na akahitaji kupata mtoto anashauriwa ashauriane na daktari wa afya ya mama na mtoto.

Maana ya shinikizo la juu la damu la mimba.

Kwa kawaida shinikizo la damu linatakiwa kua kati ya 100/60 mmhg mpaka 120/80 mmhg.  Ikiongezeka mpaka kufikia 139/89 mmhg inajulisha kwamba shinikizo la damu limeanza kuongezeka. Na litakapofika 140/90 mmhg au zaidi inaonesha kwamba shinikizo la damu limeongezeka zaidi ya wastani na inahitajika matibabu.

Hivyo basi shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito ni hali ya kuoongezeka kwa shinikizo la damu zaidi ya 140/90mmhg wakati wa ujauzito.

Hali hiyo inaweza kutokea kabla ya wiki 20 za ujauzito. Mara nyingi hii hutokea kwa wajawazito waliokua na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kabla ya kua na ujauzito. Japo hata wengine wanaweza kupata pia. Pia shinikizo hilo linaweza kuongeza baada ya wiki ya 20 ya ujauzito, ambapo ongezeko hilo mara nyingi linatokana na ujauzito wenyewe.

Aina za shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito.

Aina za shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito inatokana na mda wa kutokea ugonjwa huo, historia ya ugonjwa huo kabla ya ujauzito na madhara yanayotokana na shinikizo la juu la damu.

          Shinikizo la juu la damu la muda mrefu (chronic hypertension).

Hii hutokea kwa wale wanawake ambao walikua na tatizo la shinikizo la juu la damu kabla ya ujauzito. Na mara nyingi hutokea chini ya wiki 20 za ujauzito. Japo wakati wa wiki za mwanzo za ujauzito shinikizo la juu la damu hujificha na kuonesha shinikizo la damu kwa mjamzito lipo sawa.

            Shinikizo la juu la damu la mimba.(gestational hypertension).

Hutokea baada ya wiki ya 20 ya ujauzito na hua ndio kwa mara ya kwanza shinikizo la damu kuongezeka. Na wakati huu inakua bado kwenye mkojo hakuna protini au vitu vingine vinavoonesha madhara yanayotokana na shinikizo la juu damu kwenye mifumo/ogani za mwili hasa figo.

Shinikizo la juu la damu lisipotibiwa husababisha matatizo kwenye mifumo ya mwili. Na tatizo hilo huonekana kwa uwepo wa protein kwenye mkojo. Na hatua hiyo kitaalamu huitwa pre-eclampsia.

        Pre-eclampsia hutokea pale ambapo mama mjamzito shinikizo la damu limeongezeka baada ya wiki ya 20 ya mimba mpaka ikapelekea kupata matatizo kwenye mifumo ya mwili kama vile kuumia kwa figo,ini,damu na ubongo

Na kama shinikizo hili likifika zaidi ya 180/110 mmhg husababisha kifafa cha mimba. Ambapo huatarisha afya ya mama na mtoto.

Tafiti ya marejeo ya tafiti zilizofanyika kwenye nchi 19 barani Afrika kuanzia mwaka 2000 mpaka 2019 zilizoangalia kuenea kwa shinikizo la juu la damu kwa wajawazito na matokeo ya ujauzito. Imeonesha kwamba kuenea kwa ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kwa wajawazito(aina zote) ni kwa asilimia 8. Asilimia 0.9 ya shinikizo la juu la damu kipindi cha mimba lilisababishwa na shinikizo la juu la damu la muda mrefu,asilimia 4.1 lilitokea kwa mara ya kwanza baada ya wiki ya 20 ya ujauzito, asilimia 4.1 ya waliopata shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito walipata madhara ya ogani na asilimia 1.5 walipata kifafa cha mimba.

Wanawake wajawazito walio kwenye hatari ya kupata shinikizo la juu la damu.

        Mwanamke mwenye ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu.

Kwa sababu ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ni wa muda mrefu, kwa mwanamke mwenye ugonjwa huo akipata mimba bado atakua nao. Na kama hatopata matibabu vizuri au akachelewa kwenye kutafuta huduma mapema shinikizo la damu linaweza kuongezeka zaidi na kusababisha matatizo kwa mama kama kifafa cha mimba au kwa mtoto kwa kuzuia ukuaji wa mimba.

      Historia ya shinikizo la juu la damu kwa mimba zilizopita.

Kwa mwanamke ambae alishawahi kupata shinikizo la juu la damu kwenye mimba zilizopita anakua yupo kwenye hatari ya kupata tatizo hilo kwenye mimba zijazo.

     Wanawake wenye uzito mkubwa.

Tafiti ilofanyika Tanzania katika hospitali ya kanda ya KCMC ikiangalia uhusiano wa uzito na shinikizo la juu la damu kwa wanawake wajawazito tangu mwaka 2000 mpaka 2013, ilionesha kwamba wanawake wenye uzito mkubwa wana hatari ya kupata shinikizo la juu la damu ambalo linaweza kuleta madhara kwenye ogani za mwili ukilinganisha na wale wajawazito wasio na uzito mkubwa. Majibu hayo yanashajihiana na ripoti za sehemu nyingine duniani zinazoonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya uzito mkubwa na shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito.

Wanawake wengine waliopo kwenye hatari ya kupata shinikizo la juu la damu kipindi cha mimba ni wenye magonjwa ya figo na kisukari. Hata wenye umri mkubwa zaidi ya miaka 35 au umri mdogo chini ya miaka 20 pia wapo kwenye hatari ya kupata shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito.

Dalili za shinikizo la juu la damu la mimba.

      Kuvimba mwili.

Dalili kubwa ya shinikizo la juu la damu kwa mama mjamzito ni kuvimba mwili hasa kwenye uso au mikono. Inaweza kuonekana kwa kujaribu kama pete ya kidole inatoka kwa kawaida ua laa. Kama haitoki kwa kaiwaida kutokana na kuvimba vidole,basi huenda ikawa ni dalili ya awali ya shinikizo la juu la damu.

Shinikizo hilo la juu la damu likifika hatua ya kusababisha madhara kwenye ogani za mwili,mgonjwa atapata  dalili za mfumo wa fahamu. Ambazo ni

  • Kichwa kuuma sana.
  • Kushindwa kuona vizuri
  • Kupoteza fahamu
  • Kuhisi kichefu chefu na/au kutapika.

Na dalili nyingine zinazoashiria madhara kwenye ogani za mwili ni kama vile,

  • Kukosa mkojo
  • Kupumua kwa shida.

Vipimo vya kugundua shinikizo la juu la damu la mimba.

         Kipimo cha shinikizo la damu wakati wa ujauzito.

Kila mjamzito hupimwa shinikizo la damu kwenye mahudhurio ya kliniki ya ujauzito. Hii inasaidia kugundua kwa haraka na kumpatia matibabu husika atakaegundulika na shinikizo la juu la damu.

Baada ya kipimo cha shinikizo la damu,kama majibu ya shinikizo la damu  ni zaidi ya 140/90 mmhg, mgonjwa ataambiwa anatatizo la shinikizo la juu la damu la mimba na atapewa matibabu husika.

Japo tafiti ilofanyika na kitengo cha afya ya jamii kwenye chuo kikuu cha Dodoma mwaka 2020 inaonesha kwamba wajawazito wa vijijini hawapati huduma ya kupimwa shinikizo la damu kipindi cha ujauzito. Tatizo hilo limesababishwa na wajawazito hao kushindwa kuanza kliniki ya ujauzito mapema,kushindwa kufika kwenye mahudhurio yao kama walivopangiwa,maeneo wanayoishi,kiwango cha elimu na uwezo wa kiuchumi.

  Kuangalia uwepo wa protini kwenye mkojo.

Kipimo hiki hufanywa kwenye mkojo kwa kuangalia uwepo wa protini kwenye mkojo. Ambapo uwepo wa protein kwenye mkojo kwa kiasi cha 2+ huashiria kua shinikizo la juu la damu limesababisha madhara kwenye figo.

  Kutathmini uwepo wa dalili za shinikizo la juu la damu.

Kwenye kliniki ya wajawazito,mtoa huduma za afya atakagua na kumuuliza mjamzito kuhusu dalili za shinikizo la juu la damu zilizo  tajwa hapo awali. Kupitia dalili hizo mjamzito ataweza kugundulika kama anaugonjwa wa shinikizo la juu la damu.

Pia mjamzito atafanyiwa vipimo vya maabara ili kugundua kama mjamzito amepata madhara kutokana na shinikizo la juu la damu. Vipimo hivyo ni,

  • Kuangalia ufanyaji kazi wa aini na figo.
  • Kuangalia seli hai nyeupe za damu.

Wajawazito wote watakao gundulika na shinikizo la juu la damu watatibiwa kulingana na ukubwa wa ugonjwa huo.

Matibabu ya shinikizo la damu kipindi cha ujauzito.

Baada ya mjamzito kugundulika ana shinikizo la juu la damu,atapatiwa matibabu kulingana na aina ya shinikizo hilo.

  • Kwa wale waliokua na shinikizo la juu la damu kabla ya ujauzito na walikua kwenye matibabu, daktari atakagua dawa ili kujua kama dawa alizokua anatumia mgonjwa huyo ni salama kwake na mimba yake. Kwa sababu kuna baadhi ya dawa zinazotumika kutibu shinikizo la juu la damu lakini sio salama kwa mama mjamzito.
  • Wale wanaogundulika na shinikizo la juu la damu baada ya wiki ya 20 ya mimba watapatiwa matibabu kwa kupewa dawa za kushusha shinikizo la damu. Mgonjwa anapaswa kutumia dawa hizo kwa utaratibu aliopewa na daktari bila kuacha mpaka atakapojifungua.
  • Kama shinikizo la damu litaendelea kupanda au kutoshuka hata baada ya mgonjwa kupewa dawa. Mjamzito atalazwa kwa uangalizi wa karibu na kuangalia uwezekano wa kujifungua haraka kulingana na umri na hali ya mimba. Mara nyingi kama mimba ina wiki zaidi ya 37, na mjamzito ameanza kupata madhara kwenye ogani za mwili, mama atatakiwa ajifungue haraka pale tu shinikizo la damu litakapofika wastani baada ya kupewa matibabu ya dharura. Kama mimba ina umri chini ya wiki 34, mjamzito anaweza patiwa dawa ya kusaidia kukomaza mapafu ya mtoto.
  • Kwa mjamzito alie lazwa na akawa na dalili za kifafa cha mimba atatibiwa kwa dawa aina ya magnesium sulfate. Dawa hii husaidia kuzuia kifafa kwa mjamzito. Dozi inaweza badilishwa kulingana na hali ya mgonjwa na ufanyakazi wa figo. Kwa mjamzito mwenye tatizo la moyo kutofanya kazi vizuri atapewa dawa ya calsium gluconate badala ya magnesium sulphate.
  • Kama mgonjwa bado ataendelea kupata kifafa baada ya kupewa magnesium sulphate au calcium gluconate, anaweza patiwa diazepam ili kuzia kifafa na ataongezewa na dawa nyingine ya kusaidia kushusha shinikizo la damu kwa haraka ili kumsaidia mama aweze kujifungua pale tu shinikizo la damu litakaposhuka.

Kumbuka kuanza matibabu mapema baada ya kugundulika mjamzito kua na shinikizo la juu la damu ni bora. Kwa sababu matibabu hayo yatapunguza madhara yanayotokana na ugonjwa huo kwa mama mjamzito kama madhara kwenye ogani za mwili, kujifungua kabla ya muda, kujifungua mtoto njiti na madhara kwa mtoto kama vile ukuaji dhaifu wa mimba.

Mara nyingi shinikizo la juu la damu la mimba baada ya wiki 20 hua linashuka na kua sawa ndani ya wiki 6 mpaka 12 baada ya kujifungua. Kama bado mama atakua na shinikizo la juu la damu atapatiwa dawa ambayo haiathiri unyonyeshaji. Kwa mama aliokua na shinikizo la juu la damu kabla ya ujauzito,baada ya kujifungua anaweza kuendelea kutumia dawa alizokua anatumia mwanzo kama hazina madhara kwenye unyonyeshaji.

Dr Amanda beech na wenzake wa hospitali ya royal ya wanawake iliopo Sydney ausrtalia,wanasema kwamba dawa ya kutibu shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito ni  salama hata baada ya kujifungua. Japo kwa sababu methyldopa inachangia kusababisha msongo wa mawazo kwa asilimia 30, inashauriwa isitumike kwa mama aliejifungua. Bali itumike dawa za kundi la ACE INHIBITORS hasa enalapril ambayo kiasi chake kwenye maziwa ni kidogo na ni nzuri kipindi cha unyonyeshaji.

Madhara ya shinikizo la juu la damu la mimba.

Shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito huleta madhara kwa mjamzito mwenyewe na mimba.

     Madhara kwa mjamzito.

Shinikizo la juu la damu kwa mama mjamzito husababisha madhara kwenye ogani za mwili. Hii husababisha kuumia kwa damu, ini,figo na ubongo. Amabapo hupelekea figo kushindwa kufanya kazi na mgonjwa kupooza. Pia mgonjwa anaweza jifungua kabla ya muda,kujifungua njiti na kujifungua mtoto asiekua hai.Na kama shinikizo likizidi sana husababisha kifo kwa mjamzito.

      Madhara kwa mimba.

Shinikizo la juu la damu kipindi cha mimba husababisha upungufu kwenye mzunguko wa damu kutoka kwa mama Kwenda kwa mtoto,hali hii hupelekea ukuaji hafifi wa mtoto,mtoto kukosa hewa. Wakati mwingine placenta inaweza jiachia kutoka kwenye mji wa uzazi. Na ikifika hali hizo mtoto hupoteza uhai.

Namna ya kuzuia shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito.

  • Kwa mwanamke mwenye ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na anatarajia kupata mtoto inashauriwa kutafuta ushauri wa kitaalamu na huduma ili kujikinga na matatizo ya shinikizo hilo pindi atakapokua mjamzito.
  • Wale watakaopata shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito wapatiwe kiasi kido cha aspirine ili kupunguza uwezekano wa madhhara yanayotokana na shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito. Tafiti zinaonesha aspirine imepunguza madhara ya shinikizo la damu kwa wajawazito kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wale ambao hawakupta dawa hiyo.
  • Kujiepusha na vyote vinavoongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito kama vile uzito mkubwa. Kwa anaejiandaa kupata mimba ni vizuri kuweka sawa uzito wake.
  • Kuwahi kwenye kliniki ya wajawazito mara tu mwanamke anapojigundua ni mjamzito kunasaidia kugundua mapema ugonjwa huo na kuanza matibabu kabla ya ugonjwa kua mkubwa na kusababisha madhara mbalimbali kwa mama na kwa mtoto.

Hitimisho.

Shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito bado ni tatizo kubwa linalosababisha vifo kwa wajawazito duniani kote.

Kugundua mapema tatizo hilo wakati wa kliniki za ujauzito kunasaidia matokeo mazuri wakati wa kujifungua kwa mgonjwa huyo. Kama mgonjwa atashindwa kujifungua kawaida endapo mimba ina umri zaidi ya wiki 37, upasuaji unaweza kufanyika ili kupunguza madhara.

Ugonjwa huu unatibika. Na mama baada ya kujifungua kama atakua amepata madhara ya muda mrefu kama vile moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, anashauriwa afike kwenye hospitali yoyote iliopo karibu nae ili apatiwe matibabu zaidi.

Ukiwa Tayari! Namna 3 tunasaidia kuboresha afya yako

  1. AFYAPlans inakuwezesha Kudhibiti na kuepuka madhara ya presha: Ungana na Daktari wako kwa msaada na mwongozo binafsi Kuhusu dawa, VIPIMO, maarifa na ujuzi. Bonyeza HAPA kujiunga grupu letu.
  2. Vitabu vya Elimu vinavyokuwezesha kufanya Maamuzi sahihi kuboresha afya yako. Mfano kudhibiti kisukari huku ukila Vyakula unavyovipenda. Bonyeza HAPA kufahamu zaidi
  3. Vifaa vya Matibabu ya Nyumbani vinavyokupa amani na uhakika wa afya yako muda wote. Bonyeza HAPA kuvifahamu.

Uko tayari kuboresha AFYA Yako? Tuwasiliane

HES-P-D-BDW-1_19016

HES-P-D-SET-D8_31212

HES-WB-01_12127

HES-P-D-DM-2_22878

DM-BP-01_12034

HES-P-D-BPA-12_18778

HES-CC-D-Nebul-1_11922

HES-CC-D-PO2-1_7479

HES-P-D-SET-6_4194

Shopping Cart
Muulize Dr. Adinan
1
Muulize Dr. Adinan
Chat na Dr. Adinan
watumie na wengine wanufaike